RAIS MAGUFULI AONDOA KIGOGO MWINGINE ILUKLU
Kwa
mujibu wa mabadiliko yaliyotangazwa na Ikulu jana, Rais Magufuli
amemwondoa Ikulu Gelasius Byakanwa, ambaye alikuwa msaidizi wake wa
karibu.
Taarifa
ya iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema mpaka
mabadiliko hayo yanafanyika jana, Byakanwa alikuwa Katibu wa Rais
Msaidizi Mwandamizi.
Taarifa
hiyo iliyomnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ilisema Rais
Magufuli amempeleka kigogo huyo kuwa Mkuu wa Wilaya Hai mkoa wa
Kilimanjaro, kuchukua nafasi ya Antony Mtaka.
Katika uteuzi mpya wa wakuu wa mikoa hivi karibuni, Mataka aliteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu.
Kigogo huyo wa Ikulu anakuwa wa pili kuondolewa Ikulu baada ya Sefue aliyeondolewa katika mabadiliko yaliyotangazwa Machi 7.
Nafasi
ya Sefue ambaye alitumikia nafasi hiyo kwa miezi mitatu ya utawala wa
awamu ya tano, ilichukuliwa na Kijazi aliyekuwa Balozi wa Tanzania
nchini India.
Wakati wa mabadiliko hayo, Rais Magufuli aliahidi kumpangia kazi nyingine Sefue.
Uteuzi
wa kigogo huyo kuwa DC pia ni dalili kwamba Rais Magufuli
anakamilisha-kamilisha orodha ya wakuu wapya wa wilaya ambayo imekuwa
ikisubiriwa kwa shauku kubwa.
Watu
wengi wamekuwa na shauku ya kujua nani watarejeshwa kwenye safu hiyo
mpya na nani ambao watatupwa huku sura mpya zikitarajiwa kuonekana
kwenye utawala huo wa awamu ya tano.
Tangu
aingie madarakani, Rais Magufuli amekuwa akipunguza baadhi ya watumishi
Ikulu na kuwarejesha kwenye wizara mbalimbali walikokuwa awali.
Alipoingia
tu Ikulu Novemba 5 mwaka jana alifuta baadhi ya vitengo vilivyokuwa
Ikulu kikiwemo kile cha Lishe ya Rais na cha kukaribisha wageni binafsi.
Katika
siku zake 100 za kwanza tangu alipoingia madarakani, tayari Serikali
yake imewafukuza kazi vigogo zaidi ya 70 kwa tuhuma mbalimbali ikiwamo
za ufisadi.
Rais
Magufuli aliwang’oa vigogo wapatao 23 wa Mamkala ya Bandari (TPA) na
kuvunja Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo kutokana na upotevu wa
makontena zaidi ya 11,000.
Bodi
hiyo ilikuwa na vigogo kadhaa akiwamo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia
Ackson na Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Udhibiti ya Nishati na Maji
(EWURA), Haruna Masebu.
Hatua
ya kuvunjwa kwa bodi hiyo, ilitokana na kushindwa kuisimamia vyema
Bandari ya Dar es Salaam, hali iliyosababisha makontena 2,716 kutolewa
bandarani bila kulipia kodi na kuisababishia Serikali hasara ya
mabilioni ya shilingi.
JIPU LA RAHCO
Rais
Magufuli pia alimsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya
Rasilimali za Reli (RAHCO), Mhandisi Benhadard Tito ambaye tayari
amefikishwa mahakamani kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka.
Uamuzi
huo ulilenga kupisha uchunguzi wa kina kutokana na ukiukwaji mkubwa wa
taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya
ujenzi wa reli ya kati.
JIPU LA TAKUKURU
Rais
Magufuli pia alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hosea, Desemba 16, mwaka
jana.
Akizungumzia
uamuzi huo, aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alisema ulichukuliwa baada ya Rais Magufuli kutoridhishwa na namna
taasisi hiyo ilivyokuwa ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na
rushwa, hususani kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika bandari ya
Dar es Salaam.
Alisema
Rais Magufuli alijiridhisha kwamba utendaji kazi wa Dk. Hosea
usingeendana na kasi yake, hivyo alimteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi
Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
taasisi hiyo.
JIPU LA NIDA
Januari
26, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu ili
kupisha uchunguzi dhidi yake.
Maimu alisimamishwa pamoja na maofisa wengine wanne wa NIDA kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha za Serikali.
Maofisa
hao ni Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Joseph
Makani, Ofisa Ugavi Mkuu, Rahel Mapande, Mkurugenzi wa Sheria, Sabrina
Nyoni na Ofisa Usafirishaji, George Ntalima.
Dk. DAU wa NSSF
Magufuli alimwondoa kwenye nafasi ya ukurugenzi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau na kumteua kuwa Balozi.
MAWAZIRI
Desemba
10, mwaka jana, Rais Magufuli alitangaza baraza lake la mawaziri ambalo
alianza kwa kuteua mawaziri 19, ingawa wizara ni 18. Mawaziri sita kati
ya hao ni wanawake.
MAKATIBU NA MANAIBU
Katika
mwendelezo wa kuhakikisha kuwa wale anaowateua wanakubaliana na kasi
yake, Rais Magufuli aliwapa kiapo cha utii makatibu wakuu wa wizara na
manaibu wao.
Akiwaapisha
kiapo hicho aliwaeleza wazi kwamba yule atakayeshindwa kufanya kazi ni
bora ajiondoe mwenyewe na kupisha wengine watumikie wananchi.
AWARUDISHA NYUMBANI MABALOZI ‘MIZIGO’
Rais
Magufuli aliiagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na
Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja
mabalozi wawili ambao mikataba yao ilikuwa imemalizika.
Mabalozi
hao, Batilda Buriani aliyekuwa Japan na Dk. James Msekela aliyekuwa
Italia walitakiwa kukabidhi kazi kwa ofisa mkuu au mwandamizi aliye
chini yao.
Pia
alimrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Peter
Kallaghe na kuagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na
Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa kumpangia kazi nyingine.
NIPASHE
RAIS MAGUFULI AONDOA KIGOGO MWINGINE ILUKLU
Reviewed by The Choice
on
9:54:00 PM
Rating:
No comments: