MFANYABIASHARA MKOANI ARUSHA AKANUSHA KUHUSIKI UJAMBAZI ULIOFANYIKA MBAGALA
Mfanyabiashara
wa mjini Arusha aliyetangazwa kupitia mitandao ya kijamii akihusishwa
na ujambazi uliotokea Mbagala jijini Dar es Salaam, ameibuka na kukana
taarifa hizo na kusema zilisambazwa na washindani wake.
Tukio la majambazi kupora na kuua
katika benki ya Access tawi la Mbagala lilitokea Februari 26, mwaka huu
na watu kadhaa wanaendelea kushikiliwa na polisi.
Mfanyabiashara huyo, Ashaeri Mollel
aliliambia gazeti la Nipashe kuwa baada ya tukio hilo, washindani wake
ambao hata hivyo hakuwataja, waliisambaza picha yake kwenye mitandao ya
kijamii wakimhusisha na tukio hilo, hali iliyomsababishia usumbufu kwa
familia na marafiki zake.
“Nimekuwa nikipigiwa simu na watu
mbalimbali wakiniulizia imekuwaje nikahusika kwenye tukio hilo, sasa
inakuwa usumbufu mkubwa na wapo walioathirika kisaikolojia kutokana na
uzushi huo,” alisema.
Hata hivyo, Mollel alisema katika
siku za karibuni alitofautiana na mfanyabiashara mwenzake (jina tunalo)
wakati wakiuziana gari, hali iliyosababisha polisi kuingilia kati na
kuwapeleka kituo cha polisi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Mollel, wakiwa kwenye
gari la polisi baadhi ya watu waliwapiga picha zilizosambazwa kwenye
mitandao hiyo zikiwa na maelezo potofu kuwa alihusika na tukio la
uporaji kwenye benki.
“Ukweli ni kwamba baada ya
kufikishana polisi, kila mmoja wetu alitoa maelezo na tukaachiwa huru,
lakini cha kushangaza wenzangu wakachukua picha zile na kunizushia
kwamba nilihusika kwenye ujambazi wa Mbagala, inasikitisha ,” alisema.
Mollel ameshawasilisha malalamiko
yake Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) na kutakiwa kuwasilisha maelezo ya
awali polisi ili hatua zichukuliwe dhidi ya wahusika.
MFANYABIASHARA MKOANI ARUSHA AKANUSHA KUHUSIKI UJAMBAZI ULIOFANYIKA MBAGALA
Reviewed by The Choice
on
9:26:00 PM
Rating:
No comments: