NSSF Ndani ya Ufisadi Mzito: Wajanja Wapiga zaidi ya Sh. Bilioni 179
- Pesa iliyopigwa na wajanja NSSF ni mara tatu ya pesa iliyopigwa na wajanja wa ESCROW!
- Katika miradi yote inayosimamiwa na NSSF ya Arumeru na Kigamboni serikali imeingia hasara ya Tshs Trillioni 1.3
- Mradi wa Kigamboni wasimama, kuna ufisadi wa zaidi ya Tshs Billioni 179
- Mikataba yasainiwa kimagumashi bila kufuata sheria, wajenzi ni Waturuki.
- Ardhi ya Kigamboni ilinunuliwa kwa Tshs millioni 800 kwa ekari wakati ilitakiwa inunuliwe kwa Tshs Millioni 4.5 kwa ekari.
- Arumeru ardhi ilinunuliwa kwa Tsh Billioni 1.8 kwa ekari wakati thamani ya ekari moja ni Tshs laki 5 mpaka Millioni 1.
- Taratibu za ununuzi wa ardhi zilifanyika kimya kimya bila kumshirikisha mwanasheria wa serikali.
Mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam
uitwao Dege Eco Village, ulioanzishwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya
Jamii (NSSF) umesimama huku ikiripotiwa kuwapo kwa ufisadi wa zaidi ya
Sh179 bilioni katika mradi huo.
Mchoro wa mradi huo ulioanzishwa mwaka 2014 kwa gharama ya Dola za
Marekani 653 milioni (Sh1.3 trilioni) unaonyesha utakapokamilika
utachangia kubadili sura ya jiji la Dar es Salaam kwani kutakuwa na
nyumba za kifahari, majengo ya hoteli, maduka makubwa, eneo la wazi la
mapumziko, baa, shule, hospitali, kumbi za mikutano, nyumba za ibada na
migahawa.
Hata hivyo, mradi huo unaosimamiwa na kampuni ya Hifadhi Builders
Limited iliyoanzishwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya
Azimio Housing Estate Limited (Ahel), huku wajenzi wakiwa kampuni ya M/s
Mutluhan Construction Industry Company Limited kutoka Uturuki, huenda
usikamilike kwa muda uliopangwa kwani umesimama tangu Januari, ingawa
unadaiwa utaanza tena mwezi huu.
Ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali ameliambia gazeti la Mwananchi kwamba
ujenzi wa nyumba za Dege Eco Village ni miongoni mwa miradi ya kisasa
ambayo NSSF imekaguliwa na kubainika kufisadi fedha baada ya kuingia
mikataba bila kufuata taratibu, kanuni wala sheria za nchi.
Kwa mujibu wa ofisa huyo, ripoti ya ukaguzi iliyoishia Juni 2015,
uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)
akishirikiana na taasisi ya kimataifa ya ukaguzi ya Ernst and Young
imeanika ufisadi mkubwa unaotishia usalama wa fedha za wanachama wa
shirika hilo.
Mtoa habari huyo amesema mradi wa nyumba za kisasa wa Kigamboni
unaojengwa katika ekari 300, unakabiliwa na kashfa baada ya kubainika
kuwa NSSF imenunua ekari hizo kutoka kwa mbia mwenzake Azimio Housing
Estate Limited kwa zaidi ya Sh800 milioni kwa ekari, wakati shirika hilo
linamiliki viwanja vingine maeneo hayo vyenye thamani ya Sh4.5 milioni
kwa ekari.
“Ukipata ripoti hiyo ya ukaguzi utaweza kuona ilivyochambua miradi
mbalimbali ya ujenzi jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na
Mtwara. Kwa mfano mradi wa Arumeru mkoani Arusha, NSSF imenunua viwanja
kutoka Azimio kwa Sh1.8 bilioni kwa kila ekari,” alieleza ofisa huyo.
Uchunguzi unaonyesha kwamba Bodi ya NSSF na Azimio walitiliana saini
Novemba 15, 2013, kuhusu uendeshaji wa miradi mbalimbali. Azimio
walijieleza kuwa wanamiliki ardhi yenye ukubwa wa ekari 20,000
Kigamboni, ekari 655.3 Arumeru, ekari 7,832.7 Pwani, ekari 200 Mwanza,
ekari 5,723.6 Mtwara, na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa ujenzi wa miji
ya kisasa.
Taratibu ziliitaka NSSF kujiridhisha kuhusu uwepo wa ardhi hiyo, uhalali
wa kisheria wa Azimio kumiliki eneo hilo pamoja na thamani halisi ya
ardhi hiyo kutoka mamlaka zinazohusika. NSSF hawakufanya hivyo na wala
hawakumshirikisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
“Napenda kukuthibitishia kwamba NSSF waliridhia bila ya kujiridhisha
kuhusu uwapo wa ardhi hiyo bali walitiliana saini miradi ya pamoja
kujenga nyumba Kigamboni na Arumeru bila kujiridhisha,” alisema ofisa
huyo.
Mradi wa Kigamboni una thamani ya Dola za Marekani 653,436,675 (Sh1.3
trilioni), na mradi wa Arumeru thamani yake ni Dola 3,340,589,543 hadi
utakapokamilika.
Tatizo jingine kubwa ni kuhusu umiliki wa mradi. Uchunguzi unaonyesha
mkataba wa mradi huo uliitaka Azimio kuchangia asilimia 55 zikiwamo
ekari 300 ambazo ni sawa na asilimia 20 ya mradi, huku NSSF ikichangia
asilimia 45. Uchambuzi unaonyesha Azimio imetoa ekari 300 za Kigamboni
kwa Dola 108,906,113, na ekari 655.3 za Arumeru kwa Dola 556,764,924.
Kwa hiyo kwa miradi miwili hiyo, NSSF ‘imenunua’ ardhi yenye thamani ya Dola 665,671,037 (Sh1.33 trilioni) kutoka Azimio.
Uchunguzi unaonyesha kuwa Serikali imekasirishwa na hatua ya taasisi
hiyo ya umma ‘kununua’ ekari moja ya ardhi kwa zaidi ya Sh800 milioni
huko Kigamboni, wakati bei halisi ya ardhi iliyotangazwa na Halmashauri
ya Manispaa ya Temeke mwaka 2012 wakati ikiuza viwanja vyake ilikuwa
Sh8, 000 kwa mita za mraba, kwa hiyo ekari moja ilikuwa Sh39 milioni.
Vilevile, NSSF yenyewe ilikuwa inamiliki ekari 267 Kigamboni ilizonunua
kutoka kampuni ya Georgia Homes (T) Ltd kila moja kwa Sh4.5 milioni,
hivyo hatua ya shirika hilo ‘kununua’ ekari moja kwa Sh800 milioni
kutoka Azimio haikubaliki.
Hata mradi wa Arumeru, NSSF pia imebainika kufuja fedha kutokana na
kukubali kununua ekari moja kwa Sh1.8 bilioni, kinyume na thamani halisi
ya viwanja kwenye eneo ambalo lipo kilometa 30 kutoka Jiji la Arusha.
Uchunguzi umebaini wenyeji wa eneo hilo wanauza ekari moja kwa bei kati
ya Sh500, 000 na Sh1 milioni.
Hatua ya NSSF ‘kununua’ ekari 300 Kigamboni kila moja kwa Sh800 milioni
imesababisha hasara ya Sh179 bilioni na ekari 655.3 Arumeru kununuliwa
kila moja kwa Sh1.8 bilioni imeingiza hasara ya Sh1.165 trilioni. Kwa
hiyo, miradi miwili hiyo imeingiza hasara ya Sh1.3 trilioni.
“Tusubiri, lakini nina uhakika watu ambao kwa uzembe, walilishauri
shirika kuingia kwenye matatizo haya na kuhatarisha fedha za wanachama
lazima watawajibishwa ili kuepusha matatizo mengine yajayo kwa fedha za
wanachama wa mfuko,” alisema ofisa huyo.
Ofisa huyo alisema kwamba hadi ukaguzi ulipofanyika shughuli zote hata
manunuzi ya vitu muhimu kwa ajili ya mkandarasi zilikuwa zinafanywa na
NSSF pamoja na mawasiliano na wasambazaji wa huduma. Hadi wakati wa
ukaguzi, NSSF ilikuwa imeingiza kwenye mradi Sh205.141 bilioni na
hazikuwapo nyaraka zilizoonyesha mchango wa Azimio mbali ya ardhi.
Kauli ya NSSF
Mwananchi lilifanya juhudi kupata ufafanuzi kutoka NSSF kwa zaidi ya
mwezi moja lakini majibu hayakuridhisha. Kwanza liliambiwa shirika hilo
halikuwa na Mkurugenzi Mkuu tangu Februari 15 baada ya Dk Dau kuteuliwa
kuwa balozi.
Alipofuatwa Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Miradi wa NSSF, Yacoub
Kidula alitaka apelekewe maswali ili ajibu kwa maandishi. Alipopelekewa
maswali kwa maandishi alitaka yaandikwe kwenye karatasi yenye jina la
kampuni na namba ya kumbukumbu. Baada ya kukamilisha takwa hilo, Kidula
aliipeleka barua hiyo kwa Mhandisi Julius Nyamhokya ambaye ni Mkurugenzi
wa Hifadhi Builders.
Baada ya wiki kadhaa za kufuatilia majibu, baadaye barua ilipelekwa kwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano, Eunice Chiume ambaye alisema hawezi kuijibu
kwa kuwa bado ofisi hiyo haikuwa na mkurugenzi mkuu.
“Endeleeni kuwa wavumilivu kwa sababu sisi hatuwezi kuzungumza chochote
bila kuwa na mkurugenzi mkuu. Tukimpata atajibu kwa sababu taratibu za
ofisi zetu ni kuwa mkurugenzi mkuu ndiye mwenye majibu ya kila kitu,”
alisema Chiume.
Rais John Magufuli alipomteua, Profesa Godius Kahyarara kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa NSSF, bado majibu hayakutolewa. Chiume alisema Profesa Kahyarara
bado anajifunza mazingira ya shirika.
Mkurugenzi wa Mradi wa Kampuni ya Azimio, Vital Dege alisema mradi
unaendelea na mpaka sasa nyumba 300 tayari zimekamilika. “Mradi
haujasimama, bado unaendelea na sasa tupo kwenye hatua za mwisho,”
alisema Dege.
Lakini Mwananchi lilipotembelea eneo la mradi huo hivi karibuni,
lilishuhudia shughuli zikiwa zimesimama; walikuwapo wafanyakazi
wachache, wengi wao walinzi kutoka kampuni ya Usalama Corps na wajenzi
kadhaa wa kampuni ya Uturuki ya M/s Mutluhan. Vibarua wote, mafundi na
wataalamu mbalimbali hawakuwapo.
Walinzi wawili walionekana kwenye vibanda vya juu wakilinda majengo
yaliyobaki kama magofu. Pia, walionekana walinzi wengine wanne ambapo
wawili walikuwa kwenye lango kuu la kuingilia eneo lenye ofisi, mashine
za kutengenezea nondo na kokoto huku wengine wawili wakiwa kwenye lango
la kuingilia kwenye mradi.
“Ujenzi umesimama, kama ungekuwa unafanya kazi, nisingeweza hata
kuzungumza na wewe, ningekuwa na kazi kubwa ya kupekua watu na kukagua
magari yanayotoka nje na kuruhusu yanayoingia. Hapa pote pangekuwa
vurugu tupu, hawa wanaingia hawa wanatoka. Kule (anaonyesha kwa kidole)
kungekuwa na kelele za mashine za kokoto na nondo,” alisema mmoja wa
walinzi wawili katika lango kuu la kuingia kwenye eneo la ofisi.
“Tumebaki walinzi tu na wasimamizi wachache. Wapo wajenzi wachache Waturuki, naona nao wanasubiri kuondoka.”
Ofisa masoko wa kampuni ya Hifadhi Builders, Alphonce Kayombo aliyekutwa
eneo la mradi alisema mradi huo ulioko katika hatua ya pili ya ujenzi,
umesimama kwa muda kutokana na alichodai wajenzi kwenda likizo.
NSSF Ndani ya Ufisadi Mzito: Wajanja Wapiga zaidi ya Sh. Bilioni 179
Reviewed by The Choice
on
9:10:00 PM
Rating:
No comments: