Taarifa Fupi Kuhusu Ziara Ya Rais Wa Vietnam Nchini Tanzania Tarehe 9-10 Machi 2016
Utangulizi
Rais
wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam Mheshimiwa Truong Tan Sang
anatarajiwa kufanya ziara rasmi nchini tarehe 9 Machi 2016.
Madhumuni
ya ziara hiyo ni kukuza uhusiano baina ya Vietnam na Tanzania mbao
umedumu kwa zaidi ya miaka hamsini tangu kuanzishwa kwake pamoja
Kufungua maeneo mapya ya Ushirikiano wa kiuchumi baina ya Tanzania na
Vietnam.
Hii
ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo Barani Afrika tangu aingie
madarakani mwaka 2011, ambapo nchi nyingine anayotarajiwa kutembelea ni
Mozambique.
Rais
Truong anatarajiwa kufuatana na mke wake Bi Mai Thi Hahn, mawaziri 4
wanaoshughulika na sekta za Kilimo, Mawasiliano Uwekezaji, Afya,Viwanda
na Biashara. Aidha mgeni huyo atafuatana na ujumbe wa wafanyabiashara
30 kutoka Vietnam.
Shughuli za msingi zitakazofanyika kwenye ziara
Wakati
wa ziara hiyo Rais Truong Tang San atafanya mazungumzo rasmi na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Joseph Magufuli
Ikulu jijini Dar-es-Salaam.
Aidha,
Rais Truong pia atapata fursa ya kutembelea eneo la EPZ la Ubungo
kuangalia viwanda mbalimbali vinavyozalisha bidhaa za kuuza nje
Baada
ya kutembelea EPZA Rais Truong atahudhuria mkutano wa biashara na
uwekezaji katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere. Mkutano huo
unatarajiwa kuhudhuriwa na taasisi za umma na sekta binafsi kutoka
Tanzania na Vietnam.
Rais
Truong atamaliza ratiba yake kwa kuhudhuria dhifa ya Taifa
itakayoandaliwa kwa heshima yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dk.John Pombe Joseph Magufuli.
Wasifu wa Rais wa Vietnam
Mheshimiwa
Truong Tan Sang amezaliwa tarehe 21 January 1949 katika Jimbo la Long
An nchini Vietnam. Amepata Elimu ya Juu kutoka taasisi ya national
Academy of Public Administration ya Vietnam ambako alipata Shahada ya
kwanza ya Sanaa na Sheria.
Kutokea
mwaka 1966 hadi 1996 Mheshimiwa Truong ameshika nafasi mbalimbali za
utendaji katika Chama Tawala cha kikomunisti cha Vietnam.
Mwaka
1996 Mhe Truong alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Tawala
na Katibu wa Chama hicho katika Jimbo la Ho Chi minh hadi mwaka 2000
ambapo aliachia wadhifa wa katibu Mkuu wa Jimbo na kuendelea na nafasi
ya ujumbe wa Kamati kuu ya Chama tawala hadi tarehe 25 Julai 2011
alipochaguliwa na Bunge la Vietnam kuwa Rais wa Vietnam.
Mhe Truong amemuoa Bi mai Thi Hanh na wamejaaliwa mtoto mmoja.
Taarifa Muhimu Kuhusu Vietnam
Historia fupi ya Vietnam
Vietnam
ilifanya mapinduzi tarehe 14 Agosti 1945 na hatimaye kupata uhuru
tarehe 2 Septemba 1945 ikijulikana kwa jina la Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Vietnam.
Pamoja
na kupata uhuru nchi hiyo iliendelea kuwa na migongano baina ya Vietnam
ya Kaskazini na Kusini iliyopelekea vita iliyodumu kwa muda mrefu na
kuhusisha mataifa ya nje.
Kufuatia
kumalizika kwa vita, Vietnam ya Kaskazini na Kusini ziliungana tena na
kuunda Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam tarehe 2 Julai 1976.
Nchi
hiyo yenye kilomita za mraba 329,560 iliyopo kusini mashariki mwa Asia
ina watu milioni 91.7 na inaongozwa na Chama cha Kikomunisti cha
Vietnam.
Mafanikio ya Uchumi ya Vietnam
Vietnam ni moja ya nchi zilizopiga hatua kubwa ya maendeleo barani Asia.
Mwaka
1986 Serikali ya Vietnam ilianzisha mageuzi makubwa ya uchumi
yaliyopelekea kuitoa nchi hiyo kwenye kundi la nchi masikini yenye
kipato cha Dola za Kimarekani 100 kwa kila mtu hadi kufikia kuwa nchi
yenye uchumi wa kati yenye kipato cha Dola za kimarekani 2000 kwa kila
mtu mwaka 2014. Katika mageuzi hayo,Vietnam imefanikiwa kupunguza
umasikini wa wananchi wake kwa asilimia 50.
Mafanikio katika Sekta ya Kilimo
Sifa
kuu ya Vietnam ni uthubutu na uwezo wa kusimamia mipango yake. Mfano
mwaka 1980 nchi hiyo iliamua kuingia kwenye uzalishaji mkubwa wa
kahawa.
Ndani
ya miaka 10 iliweza kufikia uzalishaji wa tani 300,000 kwa mwaka na
hatimaye kuwa nchi inayoongoza ulimwenguni katika uzalishaji na uuzaji
wa kahawa aina ya Robuster.
Vilevile
miaka ya 1990, Vietnam ilikuwa ikiagiza mchele kutoka nje, kufuatia
hatua madhubuti walizochukua mwaka 2004 ilishika nafasi ya pili duniani
katika uzalishaji wa mchele kwa kuwa na misimu mitatu ya mavuno.
Hivi
sasa Vietnam imejiwekea malengo ya kuwa miongoni mwa wazalishaji
wakubwa wa sukari duniani ambapo mwaka 2015 uzalishaji wake umefikia
tani milioni 2 kwa mwaka.
Mbali
na mazao hayo, Vietnam inaongoza ulimwenguni kwa kuuza korosho na
pilipili manga. Vilevile,Vietnam ni miongoni mwa nchi zinazoongoza
kwenye kilimo cha muhogo na mpira.
Mafanikio
makubwa ambayo Vietnam imeyapata katika kuongeza uzalishaji katika
sekta ya kilimo, yamekuwa chachu ya ukuaji wa sekta ya viwanda ambayo
kwa sasa ndio imeshika hatamu ya uchumi wa Vietnam.
Mkakati wa Mageuzi ya Kijamii na Kiuchum 2011-2020
Aidha,
Vietnam inatekeleza mkakati wake wa kuwezesha mageuzi ya kijamii na
kiuchumi wa mwaka 2011-2020 ambao umejikita kwenye kuwapatia wananchi
elimu na stadi za ufundi kwa ajili ya kufanya kazi kwenye viwanda
vinavyotumia teknolojia ya kisasa na ubunifu; kuboresha taasisi
zinazoshughulika na masoko; na kuendelea na ujenzi wa miundombinu.
Mkakati
huo unaendana na utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa nchi hiyo ambao
kwa sasa umelenga kufanya mageuzi makubwa katika taasisi za kibenki ili
kuwezesha wananchi kupata mitaji ya kufanya shughuli za uchumi na
maendeleo; na mageuzi ya makapuni ya biashara ya Serikali ili yaweze
kushindana katika uchumi wa soko ndani na nje ya nchi pasipo kutegemea
ruzuku kutoka Serikalini.
Ni
dhahiri kwamba yapo mambo ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka
Vietnam katika safari yake ya kuwa nchi ya uchumi wa Kati ifikapo mwaka
2025. Tanzania inayo nafasi kubwa ya kuongeza uzalishaji katika mazao ya
miwa,mpunga na uvuvi kwa kupitia ushirikiano na Vietnam.
Mahusiano ya Vietnam na Tanzania
Mahusiano
ya Tanzania na Vietnam yaliyojengwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Kiongozi wa Vietnam Ho Chi Minh mwaka 1960 na
kupelekea kuanzishwa rasmi kwa mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1965. Kwa
muda mrefu mahusiano hayo yalikuwa ya kisiasa zaidi ambapo Tanzania
iliunga mkono harakati za Vietnam za kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni
kwenye ardhi yake.
Ziara za Kukuza Mahusiano za Viongozi Wakuu
Aidha
katika kipindi cha miaka 50 ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya
Vietnam na Tanzania, viongozi wa kitaifa wa nchi hizi mbili wamefanya
ziara za kudumisha mahusiano baina ya nchi hizi mbili. Tarehe 25
Septemba 1973, Rais wa Vietnam Mheshimiwa Nguyen Huu Tho alifanya ziara
nchini Tanzania.
Kwa
upande wa Tanzania, viongozi waliofanya ziara nchini Vietnam ni pamoja
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William
Mkapa (2004); Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Awamu ya Nne Mhe. Jakaya
Mrisho Kikwete (2014), Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Mhe.Dk Ali Mohamed Shein (2012); Mawaziri Wakuu wa Serikali ya
Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano Mhe.Edward Lowassa (2006); na Mhe.
Mizengo Kayanza Pinda (2010).
Mikataba ya Mahusiano baina ya Tanzania na Vietnam
Katika
jitihada za kuimarisha mahusiano, mwaka 2001 Tanzania na Vietnam
zilisaini Mkataba wa Ushirikiano wa Kuichumi na ufundi. Mkataba huo
uliainisha maeneo ya ushirikiano yafuatayo:
- Kubadilishana uzoefu katika sekta ya kilimo na maendeleo vijijini;
- Kubadilishana uzoefu katika matumizi ya sayansi na teknolojia katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na misitu;
- Kupeana taarifa za fursa za masoko ya bidhaa za kilimo
- Vietnam kuipata Tanzania utaalam na teknolojia ya uvunaji na utunzaji wa maji
- Mwaka 2014 Tanzania na Vietnam zilisaini Mkataba wa ushirikiano katika sekta ya mawasiliano ambapo kupitia mkataba huo kampuni ya Vietel inayomilikiwa na Jeshi la Vietnam imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya mawasiliano nchini na kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa watanzania 1600 na fursa za kujiajiri kwa watanzania 20,000. Vilevile,kampuni hiyo kupitia mkataba uliosainiwa,itatoa huduma za internet bure kwenye mashule na mahospitali ya Serikali vijijini.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dar es Salaam
03 Machi, 2016
Taarifa Fupi Kuhusu Ziara Ya Rais Wa Vietnam Nchini Tanzania Tarehe 9-10 Machi 2016
Reviewed by The Choice
on
12:33:00 AM
Rating:
No comments: