MAZITO YA KESI YA KAFULILA KUPINGA UBUNGE
Mahakama Kuu ya Tanzania
Kanda ya Tabora imeahirisha kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi Jimbo la
Kigoma Kusini iliyofunguliwa na aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, David
Kafulila, kupitia chama cha NCCR-Mageuzi akipinga ushindi wa Mbunge
Hasna Mwilima, wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kesi hiyo iliahirishwa jana
na Jaji wa mahakama hiyo, Ferdinand Wambali, baada ya Wakili wa
kujitegemea, Profesa Abdallah Safari, anamtetea mlalamikaji kuomba
mahakama hiyo impatie saa 48 ili akamilishe hati za kiapo za mashahidi
wake watano na baada ya hapo mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa
kwa ajili ya kuanza kusikiliza.Kafulila
Jaji Wambali alikubaliana
na ombi hilo na kusema hati za mashahidi zipelekwe kwa Naibu Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Shanmillah Sanwatt, zikiwa zimefungwa
kwenye bahasha Machi 18, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa
wa Kigoma.
Alisema siku hizi kuna
utaratibu ulioanzishwa kwamba kila shahidi lazima awe na hati ya kiapo
ndipo atoe ushahidi wake mahakamani.
Aidha, Jaji Wambali alisema
hati za ushahidi zitakuwa zimefungwa na zitafunguliwa wakati wa shahidi
anapoanza kutoa ushahidi wake.
“Nia ya mahakama ni kutatua
migogoro na siyo kuongeza migogoro, hivyo jitahidini kuwasilisha hati
za kiapo za mashahidi ili kesi hiyo isikilizwe na kutolewa uamuzi
haraka,” alisema Jaji Wambali.
Alisema kutokana na matakwa
ya kisheria, upande wa mlalamikaji unatakiwa kuwasilisha hati za kiapo
za mashahidi zikiwa zimefungwa kwenye bahasha na zifikishwe hapo
mahakamani mapema iwezekanavyo ili kesi hiyo imalizike haraka.
Jaji Wambali aliwataka mawakili wa pande zote kuhakikisha siku ya kesi kusiwapo na upande wowote kutofika hapo mahakamani.
Aidha, Jaji Wambali
aliuhoji upande wa mshtakiwa unaoongozwa na Wakili wa Kujitegemea,
Kennedy Fungamtama, kama una pingamizi dhidi ya maombi ya upande wa
mlalamikaji.
Hata hivyo, upande huo
ulidai kuwa hauna pingamizi dhidi ya maombi ya upande wa mlalamikaji na
kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa ajili ya kuanza kusikiliza kesi
hiyo.
Jaji Wambali alikubaliana
na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 29, mwaka huu kesi hiyo
itakapoanza kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kigoma.
Katika kesi hiyo, Kafulila
atawakilishwa na Wakili Profesa Abdallah Safari pamoja na Tundu Lissu,
wakisaidiana na Wakili wa Kujitegemea Daniel Rumenyela.
Kwa upande wa Mbunge
Mwilima, atawakilishwa na Wakili wa Kujitegemea, Fungamtama pamoja na
Mawakili wa Serikali wanaomwakilisha Msimamizi wa Uchaguzi na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kama washtakiwa katika kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Kafulila
anaiomba Mahakama imtangaze kuwa mshindi kwa mujibu wa Sheria ya
Uchaguzi kifungu Na. 112(c) kwa madai kwamba yeye ndiye aliyepata kura
nyingi kulingana na matokeo ya kila kituo kwenye fomu namba 21B na
kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alimtangaza Mwilima kinyume cha matokeo
halisi.
MAZITO YA KESI YA KAFULILA KUPINGA UBUNGE
Reviewed by The Choice
on
9:31:00 AM
Rating:

No comments: