Maalim Seif Aruhusiwa Kutoka Hospitali.....Asema Afya Yake Kwa Sasa Imeimarika
Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad aliyelazwa juzi katika Hospitali ya Hindul Mandal aliruhusiwa jana akisema amepona na anaweza hata kushiriki mashindano ya mbio hadi Kibaha.
Maalim Seif juzi alilazwa
katika hospitali hiyo baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye ndege
akitokea Zanzibar kuja Dar es Salaam na aliondoka hospitalini hapo jana
saa 12.30 jioni.
Akizungumza wa waandishi wa habari, makamu huyo wa
kwanza wa Rais wa Zanzibar alisema madaktari wa hospitali hiyo
wamemhudumia vizuri na alianza kupata nafuu baada ya saa tatu, tangu
alipofikishwa hospitalini hapo
“Kama
mnavyoniona niko ‘fit’, nimelala usingizi mzuri leo na hali yangu
imerudi kama kawaida, naweza hata kufanya mashindano ya kukimbia,” alisema
baada ya kuteremka kutoka ghorofa ya tatu alikolazwa hadi chini kwa
lengo la kuwaeleza waandishi wa habari kuhusu afya yake.
Maalim
Seif ambaye alikuwa akitembea kwa ukakamavu, alisema amejisikia faraja
baada ya watu wengi kutaka kufahamu maendeleo ya afya yake.
“Watanzania
na Wazanzibari waliopo ndani na nje ya nchi wameonyesha mahaba makubwa
kwangu kwa namna wanavyoendelea kufuatilia afya yangu, ninawashukuru
sana,” alisema.
Akisimulia
namna alivyougua, Maalim Seif alisema hali yake ilianza kubadilika
akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar akielekea Dar es Salaam.
“Nilitoka
nyumbani jana (juzi) nikiwa mzima wa afya, baada ya kuugua ghafla
uwanja wa ndege, niliamua kuendelea na safari kwa kusaidiwa na wasaidizi
wangu. Tuliamua kuja Hindu Mandal kwa ajili ya vipimo na matibabu,” alisema.
Alisema madaktari waliamua alale hospitali hapo ili akupata uangalizi wa karibu.
Kuhusu safari yake ya India, alisema; “namshukuru Mungu nimerudi salama na Ijumaa iliyopita nikapata mapokezi makubwa Zanzibar. "
Daktari
wa Maalim Seif, Dk Omar Suleiman alisema makamu huyo wa Rais, alipata
kizunguzungu na madaktari walipomfanyia uchunguzi hawakuona ugonjwa
wowote hivyo walisema kizunguzungu hicho kilitokana na uchovu.
“Kwa
hiyo matibabu na kusafiri muda mrefu kutoka India hadi Zanzibar,
alihitaji muda mrefu wa kupumzika, nadhani ndiyo maana amepata
kizunguzungu,” alisema.
Kama
ilivyo kawaida kwa viongozi mbalimbali kutembelea wenzao wanapokuwa
hospitali, jana ilikuwa tofauti kwa Maalim Seif baada ya kutoonekana
kiongozi yeyote wa Serikali ya Zanzibar wala wa Muungano.
Viongozi
waliomtembea ni wa CUF, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Nassor Ahmed Mazrui
na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Ismail Jussa.
Maalim Seif Aruhusiwa Kutoka Hospitali.....Asema Afya Yake Kwa Sasa Imeimarika
Reviewed by The Choice
on
6:47:00 AM
Rating:
No comments: