Hivi ndivyo Chadema yachambua siku 120 za Magufuli, Wametaja mapungufu haya

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezichambua siku 120 za Rais John Magufuli tangu ashike wadhifa huo kikidai kuwa uongozi wake umetawaliwa na ukiukwaji wa haki, demokrasia na utawala bora.

Aidha, Kamati Kuu ya chama hicho iliyokutana hivi karibuni imeitisha mkutano wa Baraza Kuu utakaofanyika Machi 13 jijini Mwanza ambao utatoa msimamo wa jinsi chama hicho kikuu cha upinzani kitakavyoidai haki badala ya kuiomba na kuweka mkakati wake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Kasoro zilizotajwa kushikia hatamu katika siku hizo zilizotimia jana ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuendesha uchaguzi kwa upendeleo na haki kutotendeka Zanzibar baada ya kufutwa kwa uchaguzi, kuingiliwa kwa uchaguzi wa wenyeviti wa halmashauri na mameya, kuthibiti Bunge na uundwaji wa kamati na viongozi wake, polisi kuzuia mikutano ya hadhara na wabunge na madiwani wa Chadema kukamatwa kwa sababu zisizo za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maazimio ya kikao hicho, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliitaka mamlaka husika kutangaza tarehe ya uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam, siku saba kabla ya kufanyika kwake.
“Hatutaomba tena kumpata meya wa Jiji la Dar es Salaam, tutadai kumpata. Serikali isifikiri wao ndiyo wanapanga tarehe. Mara nyingi wamekuwa wakitushtukiza ila kwa mujibu wa kanuni tarehe inapaswa kutangazwa siku saba kabla ya uchaguzi. Siku hiyo tutachagua meya na kama asipochaguliwa tusilaumiane,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, demokrasia imekuwa ikikua kwa kasi licha ya kuwa na changamoto kadhaa lakini miezi minne ya utawala wa Rais Magufuli, demokrasia hiyo inatoweka taratibu.
Kuhusu uchaguzi wa Zanzibar, alisema wagombea walioshinda kihalali kwa kupigiwa kura na wananchi hawakupewa fursa ya kuongoza jambo ambalo linaweza kuathiri masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutawala ndani ya nchi.
Akizungumzia Bunge, Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema kumekuwa na udhibiti wa mhimili huo kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, kisheria na kikanuni wa kuisimamia Serikali na jambo hilo limefanyika katika maeneo matatu; kuzuia urushwaji wa matangazo ya moja kwa moja ya kupitia Televisheni ya Taifa (TBC), jambo alilodai kuwa limefanywa kibabe na Serikali ya CCM bila kujali kuwa “televisheni hiyo ni mali ya wananchi siyo chama tawala.
“Aidha, Serikali ya CCM imeingilia kwa kiwango kikubwa uundwaji wa uongozi wa kamati za Bunge zinazosimamia fedha za umma. Hapa kuna (Hesabu za Serikali) PAC na (Hesabu za Serikali za Mitaa) Laac,” alisema Mbowe.
Alisema kamati hizo zinapaswa kuongozwa na Kambi ya Upinzani Bungeni lakini CCM ilijiwekea utaratibu wa kuwapangia wapinzani viongozi wa kuongoza kamati hizo mbili.
“Tunastahili kuwa na mamlaka kamili ya kuchagua viongozi wa kamati hizi. Serikali pia imedhibiti uundwaji wa kamati za Bunge... Katika Bunge hili, Serikali na uongozi wa Bunge wametengeneza kamati bila kuthamini ujuzi, uzoefu na taaluma za wabunge. Hii itafanya Bunge kukosa meno,” alisema Mbowe.
Alidai kuwa polisi kwa maelekezo ya Serikali, imezuia mikutano ya siasa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu. Alisema mikutano inayoruhusiwa ni ya wabunge tu, si ya viongozi wala vyama vya siasa ambavyo vinahitaji kushukuru wananchi baada ya kumalizika kwa uchaguzi.
“Leo ni miezi minne baada ya uchaguzi bado tunazuiwa kufanya mikutano. Licha ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kulitolea ufafanuzi suala hili bado tunazuiwa kufanya mikutano,” alisema Mbowe.
Alisai kuwa polisi imewafungulia mashtaka viongozi mbalimbali wa Chadema, wakiwamo wabunge na madiwani kwa kudai masuala ya msingi kuhusu haki zinazokiukwa.
Alisema mkutano wa Baraza Kuu utakaokuwa na wajumbe zaidi ya 600, wakiwamo wabunge na wenyeviti wote wa chama hicho utatoa msimamo na mwelekeo.
Akitolea mfano wa uchaguzi wa meya wa Jiji la Dar es Salaam alisema: “Kuongoza Dar es Salaam si mapenzi ya Mbowe ni wananchi. Woga kwetu ni mwiko na kauli ya amani bila haki haiwezekani. Tunaiambia Serikali na dola kwamba amani itapatikana tukiheshimiana na haki kuchukua mkondo wake kwa kufuata utawala wa sheria na Katiba.”
Alipoulizwa kuhusu madai ya Chadema, Waziri wa Habari, Nape Nnauye aliwataka viongozi wa chama hicho kutangaza hadharani kuwa wanamkubali Rais Magufuli kabla ya kuchambua siku 120 za utawala wake.
“Hawa Chadema walimkataa Magufuli, walisema hawamtambui na hata bungeni walimsusia, leo wanawezaje kuchambua kazi zake?” alihoji Nape.
Nape ambaye pia ni Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema Watanzania wanajua kazi nzuri ya Dk Magufuli na kuwataka Chadema wauchambue utawala wake baada ya kumkubali.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene alisema haoni kama kuna ukiukwaji wa haki za binadamu katika utumbuaji wa majipu kwani umelenga kusaidia wananchi wa hali ya chini.
“Hata hivyo, kama kuna anayeona ameonewa hajazuiwa kwenda mahakamani kupinga na kupata haki yake. Ni lazima Serikali ifanye kazi yake,” alisema.
Kuhusu umeya, Mwambene alisema CCM haina kosa katika hilo, bali inafuata kanuni na taratibu akisema Chadema inajua kilichotokea na inachofanya sasa ni kutafuta visingizio tu na wala si kingine.
“Mbona waliposhinda umeya Ubungo CCM hawakuenda mahakamani? Waache taratibu zifanye kazi,” alisema
Hivi ndivyo Chadema yachambua siku 120 za Magufuli, Wametaja mapungufu haya Hivi ndivyo Chadema yachambua siku 120 za Magufuli, Wametaja mapungufu haya Reviewed by The Choice on 8:09:00 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.