JESHI LA POLISI LAOMBA MSAADA KUTOKA JESHI LA JWTZ KUSAIDIA VITA DHIDI YA MAJAMBAZI
Siku
moja baada ya majambazi kuvamia Benki ya Access Tawi la Mbagala Rangi
Tatu, kuua watu watatu akiwamo Polisi na kujeruhi watu wengine watatu
akiwamo polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga amesema
wataomba msaada wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) ili kukabiliana na matukio
ya ujambazi.
Alisema Jeshi la Polisi linajipanga upya kuhakikisha wananchi wanakuwa na amani kwa kuwashughulikia majambazi popote walipo.
Waziri
Kitwanga alisema wanaanza na Mkoa wa Pwani, kwa kuhakikisha wanawasaka
na kufyeka mapori yote ya Bagamoyo na kwingineko ili kuvunja mtandao
wao.
“Kama
walidhani Jeshi la Polisi limelala lipo macho, walichofanya ni kama
wamemuamsha aliyelala, tutawasaka, tutawakamata na tutawapeleka kwenye
mkono wa sheria na tutahakikisha tunawamaliza wote,” alisema Kitwanga.
Alisisitiza kuwa wanaotumia pikipiki
nguvu ya ukaguzi itaongezwa dhidi ya vyombo hivyo, kwa sababu inaonekana
wahalifu wengi hasa majambazi hutumia usafiri huo kutekeleza uovu wao.
Akielezea
tukio la uporaji wa Mbagala, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam, Simon Sirro alisema wamefanikiwa kuwaua majambazi watatu kati ya
12 waliofanya uvamizi huo.
Alisema
majambazi hao walikufa baada ya kupigwa risasi katika majibizano ya
risasi na Polisi katika Kijiji cha Chui Mkuranga, baada ya kujaribu
kutoroka walipozidiwa nguvu.
Alisema majambazi hao wakiwa na
pikipiki sita, huku kila moja ikiwa na majambazi wawili waliokuwa na
bunduki aina ya SMG na mabomu ya kutupa kwa mkono, walivamia benki hiyo
na kuwashambulia kwa risasi kisha kuwajeruhi wafanyakazi wa benki hiyo
waliokuwa katika chumba cha kuhifadhia fedha.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Salum
Juma na Francis Amani, na kupora kiasi cha fedha kinachokadiriwa kuwa
kati ya Sh20 na 30 milioni za kaunta baada ya kushindwa kuvunja chumba
cha kuhifadhia fedha.
Alisema kabla ya kuingia ndani,
walivamia kibanda cha walinzi na kumpiga risasi askari mwenye namba
H7739PC Khalid Juma ambaye alifariki dunia papo hapo.
Pia, walimjeruhi kwa kumpiga risasi
kwenye nyonga askari Shaban, ambaye amelazwa katika Hospitali ya
Muhimbili na kupora bunduki mbili.
Kamanda Sirro alisema majambazi hao
baada ya kufanya uporaji walipokuwa wanaondoka, walifyatua tena risasi
iliyompata kidevuni na kumuua papo hapo Abdi Salum, ambaye ni muuza duka
jirani na benki hiyo na Baraka Fredrick, mlinzi wa kampuni ya Security
Group of Africa.
“Hata hivyo Polisi wamefanikiwa
kukamata bunduki tatu kati ya hizo mbili ni mali ya Polisi, mabomu
matatu ya kutupa kwa mkono na pikipiki sita zilizokuwa zikitumiwa na
majambazi hao walipozidiwa nguvu walizitelekeza na kukimbia,” alisema
Sirro.
Katika hatua nyingine, Februari 18,
eneo la Kiwalani polisi walikamata majambazi watatu wakiwa na bastola
moja na Februari 24 eneo la Upanga karibu na Daraja la Sarender, askari
waliwakamata watuhumiwa watatu kwa makosa ya kujihusisha na ujambazi wa
kutumia silaha.
Kamanda
Sirro alisema baada ya kuwahoji walikiri kufanya matukio ya ujambazi wa
kutumia silaha na kumtaja mtuhumiwa mwenzao mmoja anayeishi Tabata
Kinyerezi jijini Dar es Salaam.
“Alipofuatwa nyumbani kwake, alikutwa na sare za jeshi hilo, redio ya upepo na pingu,” alidai kamanda huyo.
JESHI LA POLISI LAOMBA MSAADA KUTOKA JESHI LA JWTZ KUSAIDIA VITA DHIDI YA MAJAMBAZI
Reviewed by The Choice
on
10:22:00 AM
Rating:
No comments: