POLISI ANAYEMILIKI NYUMBA 40 ANG’OLEWA, SUZAN KAGANDA ARITHI MIKOBA YAKE
Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu
Mkuu
wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu, amemwondoa kwenye nafasi yake,
Mnunuzi wa Vifaa na Boharia Mkuu wa jeshi hilo, Naibu Kamishna wa Polisi
(DCP), Adriano Magayane ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.
Kuondolewa
kwa DCP Magayane katika nafasi hiyo kunatokana na taarifa
zilizochapishwa na vyombo vya habari hivi karibuni, kuwa anamiliki
nyumba zaidi ya 40 na kumbi kadhaa za starehe ndani na nje ya Dar es
Salaam.
Kwa
mujibu wa Gazeti la Mtanzania, IGP Mangu amefikia uamuzi huo kwa kile
kinachodaiwa kuwa tuhuma hizo ni nzito na zinalenga si kumfedhehesha
yeye kama ofisa mkuu wa Jeshi la Polisi, lakini kwa jeshi zima.
“IGP
Mangu amemwondoa mara moja DCP Magayane kutokana na tuhuma
zinazomkabili, kwa kweli ni nzito, nadhani hatua zilizochukuliwa ni
sahihi… unajua sisi askari tuna miiko ya utendaji kazi, sasa inapotokea
tuhuma kama hizi kwa ofisa kama huyu, lazima uchunguzi wa kina
ufanyike,” kilisema chanzo .
Kilisema
kuwa uchunguzi dhidi ya ofisa huyo unafanywa na Ofisi ya Mkurugenzi wa
Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Diwani Athumani.
Katika
mabadiliko hayo, habari za ndani zinasema kuwa DCP Magayane
amehamishiwa Makao Makuu ya Polisi, Kitengo cha Uzuiaji wa Makosa.
Alipoulizwa ana, IGP Mangu alikiri kumwondoa ofisa huyo, lakini hakueleza amepangwa kitengo gani.
“Ni
kweli nimemwondoa kwenye nafasi yake jana (juzi) ili kupisha uchunguzi
wa suala hili kwani ni zito, lazima tujiridhishe kabla ya kuchukua hatua
zaidi,” alisema.
Alipoulizwa
ni nafasi gani ambayo atapewa DCP Magayane baada ya kuhamishiwa Makao
Makuu ya Polisi, IGP Mangu alisema jeshi hilo lina kazi nyingi hivyo
atapangiwa majukumu mengine bila kuingia kwa undani.
Aidha,
IGP Mangu alisema ameagiza uchunguzi wa tuhuma hizo zilizotolewa kwenye
vyombo vya habari, uanze mara moja ili wajiridhishe kabla kuchukua
hatua zaidi.
Pamoja
na uamuzi huo wa IGP Mangu, tayari vyombo vya dola vimeanza kumuhoji
DCP Magayane, ikiwamo kumtaka awasilishe nyaraka zinazohusu umiliki wa
mali zake zote.
Kutokana
na hali hiyo, IGP Mangu amelazimika kufanya mabadiliko madogo ndani ya
jeshi na kumteua Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Suzan Kaganda
kushika nafasi ya DCP Magayane.
ACP
Kaganda amewahi pia kuwa msaidizi wa Boharia Mkuu miaka kadhaa
iliyopita kabla ya kuwa msemaji wa Jeshi la Polisi mwaka 2007 hadi 2008,
baada ya kustaafu kwa aliyekuwa msemaji, ACP Abdallah Msika.
Mbali
na kushika wadhifa huo, ACP Kaganda aliwahi pia kuwa Ofisa Mnadhimu wa
Polisi Mkoa wa Dodoma na baadae kuteuliwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Dodoma ambako alihudumu kwa miaka miwili kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa
Tabora.
POLISI ANAYEMILIKI NYUMBA 40 ANG’OLEWA, SUZAN KAGANDA ARITHI MIKOBA YAKE
Reviewed by The Choice
on
6:00:00 AM
Rating:
No comments: