Ofisi ya Bunge Yalivaa Gazeti la Nipashe....Yalitaka Liombe Radhi


Ofisi ya Bunge imebaini upotoshwaji mkubwa Katika habari iliyochapishwa na Gazeti la Nipashe toleo la Aprili 16, 2016 yenye kichwa cha habari kisemacho “ Bunge sasa laufyata mkataba wa Lugumi”. 
Habari hiyo imeandikwa kufuatia ufafanuzi uliotolewa na Bunge jana kuhusu maagizo yaliyotolewa na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) dhidi ya utekelezaji wa mkataba wa Jeshi la Polisi na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd  kuhusu mradi wa utambuzi wa alama za vidole (AFIS) (Automated Fingerprint Identification System.)
 
Ndani ya habari hiyo pia, Gazeti hilo limeeleza kuwa kamati ya PAC iliwahi kuliandikia Jeshi la Polisi kulitaka liwasilishe mkataba huo mbele ya Kamati, jambo ambalo si kweli bali ni upotoshwaji wa makusudi wenye lengo la kujenga hisia mbaya kuhusu mwenendo wa shughuli za Bunge mbele ya Umma.
 
Ukweli ni kwamba PAC haijawahi kuliandikia jeshi la Polisi kama inavyodaiwa na Gazeti hilo. Nukuu ya  maelezo ya PAC katika Hansard kwa Afisa Masuhuli kuhusu jambo hilo inasema kama ifuatavyo:
 
“Kamati inamuagiza Afisa Masuhuli kuwasilisha maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa Mkataba baina ya Jeshi la Polisi na  Kampuni ya Lugumi Enterprises  kuhusu mradi wa AFIS. Maelezo hayo yawasilishwe kwa Ofisi ya  Katibu wa Bunge kabla ya Jumatatu tarehe 11 Aprili, 2016”.
 
Katika agizo hilo PAC haikuwa imeandika kwa maandishi kuhusu agizo lake hilo hadi tarehe 12 Aprili, 2016 ilipo mweleza Katibu wa Bunge aweze kuwasilisha agizo hilo kwa maandishi ili liweze kupata Kinga chini ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ambapo barua iliandikwa na kuwasilishwa kwa Afisa Masuhuli ili kupatiwa maelezo hayo kabla ya tarehe 18 Aprili, 2016.

Aidha, Mwandishi pia amelituhumu Bunge kuwa lina nia ya kuficha ukweli kuhusu jambo hili kwa kusema   taarifa ya ufafanuzi iliyotolewa na Bunge ni “kama kufunika kombe mwanaharamu apite kwa kujaribu kupotosha maagizo ya yaliyotolewa na kamati ya PAC ambayo inataka kuuona mkataba huo”

Ni vyema ikafahamika kuwa si jambo jema kwa mwandishi au chombo chochote cha habari kulituhumu Bunge linapotekeleza majukumu yake kwa kuwa Bunge linafanya kazi zake kwa kwa kuzingatia kanuni zake za Kudumu ikiwa ni pamoja na Sheria.  
 
Ofisi ya Bunge inalisihi Gazeti la Nipashe kuomba radhi kutokana na taarifa yake hiyo iliyojaa upotoshwaji mkubwa kwa uzito ule ule au kurekebisha taarifa yake kulingana na ukweli ulivyo haraka iwezekanavyo.

Imetolewa na;
Ofisi ya Bunge,
Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano,
S.L.P 9133,
DAR ES SALAAM.
16 Aprili, 216.
Ofisi ya Bunge Yalivaa Gazeti la Nipashe....Yalitaka Liombe Radhi Ofisi ya Bunge Yalivaa Gazeti la Nipashe....Yalitaka Liombe Radhi Reviewed by The Choice on 10:33:00 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.