Kigogo wa TBC ‘Ajimilikisha’ kiwanja cha shirika.....Naibu Waziri Ampa Siku 7 za Kujieleza

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, ametoa siku saba kwa Meneja Rasilimali Watu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Neema Mrindoko kujieleza sababu za kuandika jina lake katika kiwanja cha shirika kilichopo Kisarawe mkoani Pwani.

Wambura alitoa agizo hilo juzi alipotembelea kiwanja hicho kilichopo eneo la Kimani ambacho mpaka sasa hakijakamilisha usajili wake na kupewa hati wakati kilinunuliwa na shirika hilo mwaka 2012. 
Kiwanja hicho kimejengwa nyumba za watumishi ambao wangekuwa wakifanya kazi katika kituo cha Kisarawe lakini hazijakamilika.

“Natoa siku saba, mtu huyu awe amenipa maelezo ya kutosha kwa nini hati hiyo imesainiwa na mtu mmoja ambaye ni yeye na ameandika jina lake badala ya jina la Shirika, ina maana alikuwa hajui? Hii ni makusudi,” alisema Wambura.

Wambura alisema mtu huyo amefanya makusudi kwa nafasi yake kushindwa kutambua kukaa miaka yote hiyo bila kupewa hati na kutelekezwa bila kuendelezwa ni ufisadi ambao hauwezi kuvumiliwa.

Awali Wambura alipokuwa akipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa wilaya hiyo, Mwanamvua Mrindoko, alisema kiwanja hicho chenye meta za mraba 9,567 kilipimwa na kusajiliwa kwa namba 68,480 mwaka huo huo shirika liliomba kuandaliwa hati.

Mrindoko alisema utaratibu wa ukamilishaji hati ulifanyika na walilipia na kujaza fomu ya maombi ya hati. Ilielezwa kwamba, baada ya TBC kuisaini na kuirudisha Wizara ya Ardhi ilionekana kuwa na upungufu ikarudishwa.

Alitaja upungufu huo kuwa ni hakukuwa na nakala halisi ya kuanzishwa shirika na pia fomu hiyo ilisainiwa na mtu mmoja badala ya wahusika wawili wa TBC na hivyo kukwamisha mchakato wa kupata hati.

Naibu Waziri huyo alipomhoji Ofisa miradi wa wizara hiyo, Macksselin Chota ambaye alikuwepo kwenye ziara, alisema maelezo hayo ni sahihi na kwamba upungufu wanaufanyia kazi. Chota alisema viwanja vingi vya TBC havijapata hati.

Kati ya viwanja 55, viwanja 19 pekee ndivyo vyenye hati. Alisema pia viwanja vingi viko katika migogoro mbalimbali kama vile uvamizi na pia uporaji. Naibu Waziri Wambura aliagiza ndani ya siku hizo saba hati ya kiwanja hicho cha Kisarawe iwe imepatikana.

Alitaka shirika pia lieleze ni namna gani watafanya kuendeleza majengo ambayo yameanza kujengwa hapo. 
“Hii inatia mashaka kabisa, mnachelewesha kupata hati na baadaye viwanja vinaingia kwenye migogoro, unafanya hivyo ili baadaye nyie wenyewe mzunguke, tutashindwaje kuamini hivyo?” Alihoji Naibu Waziri
Kigogo wa TBC ‘Ajimilikisha’ kiwanja cha shirika.....Naibu Waziri Ampa Siku 7 za Kujieleza Kigogo wa TBC  ‘Ajimilikisha’ kiwanja cha shirika.....Naibu Waziri Ampa Siku 7 za Kujieleza Reviewed by The Choice on 7:05:00 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.