Wafanyakazi 597 Waliosimamishwa Kazi NIDA Waandamana Kudai Haki Zao
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wameandamana
kupinga kitendo cha mamlaka hiyo kuvunja mikataba yao huku wakidai
mishahara ya miezi mitatu.
Wafanyakazi hao walichukua hatua hiyo jana,
siku moja baada ya Kaimu Mkurugenzi wa Nida, Dk Modestus Kipilimba
kutangaza kuvunja mikataba ya wafanyakazi 597 kwa sababu ya ufinyu wa
bajeti na kuongeza ufanisi katika mamlaka hiyo.
Alipoulizwa kuhusu madai
hayo, Dk Kipilimba alikiri wafanyakazi kudai mishahara yao ya miezi
mitatu na kuwa ameshapeleka maombi ya fedha serikalini na muda wowote
watawalipwa stahiki zao.
Wafanyakazi hao walisema mkurugenzi huyo
amefanya uamuzi huo kwa kukurupuka bila kukaa nao na kuzungumza jinsi
gani watalipwa stahiki zao kabla ya kuvunjwa kwa mkataba huo.
Mtaalamu
wa takwimu, Joseph Mtitu alisema alishangazwa na taarifa za kuvunjiwa
mkataba wake wakati anadai mishahara ya miezi mitatu.
Kijana huyo ambaye
alikuwa anafanya kazi ya kuingiza taarifa za wananchi kwenye mfumo wa
data, alisema mkurugenzi amefanya kazi na vyombo vya habari badala ya
kukaa na wafanyakazi wake.
“Hajafuata taratibu, alitakiwa kutupa taarifa na kuhakikisha kwamba anamaliza madeni yote ndipo avunje
mikataba... hatumuelewi,” alisema Mtitu.
Kijana huyo alisema waathirika
wengi kati ya waliovunjiwa mikataba ni vijana ambao wengine wana familia
zao akisema kitendo hicho kinaweza kusababisha baadhi yao kujiingiza
kwenye vitendo vya ujambazi na ukahaba ili kuendesha maisha yao.
Mfanyakazi mwingine, Bhoke Mafube alisema Nida imekuwa ikiwakata fedha
za mifuko ya jamii ambako walijiandikisha, lakini wakienda kuuliza huko
wamekuwa wakiambiwa wao si wanachama na fedha zao hazipo.
Akizungumzia
sababu ya ufanisi mdogo, Peter Michael alisema tatizo hilo siyo lao,
bali ni ufinyu wa rasilimali uliosababishwa na uongozi wenyewe.
Hata
hivyo, alisema hiyo si sababu ya kukiuka taratibu na haki za
wafanyakazi kwa kuvunja mikataba yao kwa kuwa wamekuwa wakifanya kazi
katika mazingira magumu.
“Tumekuja hapa viongozi hawataki kuzungumza,
sijui tutafikiaje muafaka kama wanafanya hivi.
Sisi siyo watoto wadogo,
madai yetu ni ya msingi. Watulipe mishahara yetu ndiyo tuanze kujadili
uhalali wa kuvunja mkataba,” alisema mfanyakazi huyo wa Nida.
Akifafanua
madai hayo, Dk Kipilimba alisema mamlaka yake haina fedha kwa sasa
ndiyo maana ameamua kuvunja mikataba ya wafanyakazi hao. Alisema njia
pekee ilikuwa ni kuvunja mikataba hiyo ili deni lisiendelee kuongezeka.
Alisisitiza kwamba haki ya mtu haipotei na kuwa atasimamia kikamilifu
suala hilo ili kila mfanyakazi apate haki yake.
“Ni kweli kwamba
wafanyakazi hao hawakulipwa mishahara yao ya miezi mitatu kwa sababu
hakuna fedha. Nitahakikisha wanalipwa fedha hizo lakini kwa sasa hakuna
kazi.
Hebu fikiria, tuna kompyuta 150 tu wakati wafanyakazi hao wako
597, hatuwezi kwenda,” alisema Dk Kipilimba.
Mkurugenzi huyo aliongeza
kuwa lengo la mamlaka yake ni kutengeneza vitambulisho vya kila
mwananchi na siyo kutoa ajira kwa watu hata kama hakuna kazi za kufanya.
Wafanyakazi 597 Waliosimamishwa Kazi NIDA Waandamana Kudai Haki Zao
Reviewed by The Choice
on
7:14:00 AM
Rating:
No comments: