Magufuli Asema Mafisadi Wakimshinda Asiitwe Rais
Rais
Dk. John Magufuli amesema amejitolea kuwa sadaka kwa Tanzania katika
vita dhidi ya mafisadi na kwamba akishindwa kufanya hivyo, hakuna sababu
ya yeye kuitwa rais.
Pia amesema wote waliotumbuliwa majipu watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Akizungumza
jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika sehemu ya barabara
ya Sakina hadi Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1, itakayokuwa na
njia nne, alisema ataendelea kutumbua majipu kwa kuwa wanaonufaika na
kudidimiza uchumi wa nchi ni wachache.
“Tumeanza
kuchukua hatua ndogo ndogo, tunatumbua majipu. Mpaka sasa
waliotumbuliwa si wengi kiasi hicho, hawajafika hata 2,000. Juzi juzi
nimesikia baadhi ya watu wameanza kuwatetea wanaotumbuliwa, nasema hao
wanaowatetea washindwe na walegee,” alisema.
Hafla
hiyo ilihudhuriwa pia na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta
wa Kenya, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu
wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Igga, Balozi wa Japan nchini
na mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Alisema
wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida na taabu
kutokana na wachache kufilisi mali na rasilimali za nchi.
“Ifike
mahali mmoja lazima ajitolee kufanya kazi hii. Mimi nimeamua kuwa
sadaka kwa Tanzania, lazima tufanye kazi ya kutumbua majipu na kuwaletea
maendeleo wananchi.
“Nisipofanya
hivyo, hakuna sababu ya mimi kuitwa Rais. Hii nasema kwa dhati kabisa
kutoka moyoni mwangu, naomba Watanzania waniombee,”alisema.
Alisema
kwa mfano yapo mambo ya hovyo ambayo hivi karibuni Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeisababishia serikali upotevu wa fedha za
matumizi ya simu nje ya nchi husika (roaming) kiasi cha Sh. bilioni
200.
Alisema watu wote wanaojihusisha na ufisadi watafukuzwa na kufikishwa mahakamani mwishowe kufungwa ili nao wakapate machungu.
“Hii
nchi ilifika mahali ikawa kama shamba la bibi vile,” alisema na
kusisitiza kuwa katika kuwaletea wananchi maendeleo hatafanya ubaguzi
wowote kwa kuzingatia vyama, dini, kabila ila atachapa kazi tu.
“Nawaomba
Arusha tujenge umoja wetu, tusibaguane. Tukianza kujenga umoja wa
Tanzania na tukaunganishaa na umoja wa Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na
Sudan Kusini, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na maendeleo ya
kasi," alisema Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Aliongeza kuwa: "Tukiamua tunaweza kubadilika na kuwaletea wananchi wa jumuiya hii maendeleo makubwa.”
Alisema
wananchi wa EAC wanachohitaji si vyama ila kazi, maendeleo na maisha
mazuri na si kuwafanya wachache wawe wanafaidi kuliko wengine.
Awali, alimpongeza Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kwamba ni mtu mchapakazi.
“Nampongeza sana Nassari, ni kijana safi anachotaka ni kazi na ameweza kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.
"Sipendi kuwa mnafiki, nampongeza sana Nassari. Ukimtazama usoni Nassari ni Chadema lakini kwa kweli moyo wake uko CCM,” alisema na kufanya umati wa watu kulipuka kwa shangwe.
Mapema Rais Museveni alisema: “Tukiwa tunazungumzia uchumi wa kisasa, Afrika hakuna umaskini, ina utajiri mwingi wa raslimali isipokuwa inakosa maendeleo tu.
“Ardhi ipo, madini yapo, lakini tunashindwa kuzitumia, hivyo tunakosa maendeleo, tunakosa elimu na tuna afya duni,” alisema.
Aliwataka wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa badala ya kulimia tumbo peke yake.
Museveni alisema sekta ya kilimo, viwanda, huduma na ICT, ndizo zinazoweza kuleta maendeleo kwa nchi za EAC.
Hata hivyo, alisema shida ya Waafrika ni kulala na kwamba wanalala huku kukiwa kumekucha na kusisitiza kuwa:
“Tukiamka sisi sote tutakuwa na maendeleo kutokana na uzalishaji mkubwa utakaokuwapo," alisema.
Aliwaondoa
wananchi hofu ya kupatikana kwa soko pale aliposema jumuiya hiyo ina
watu zaidi ya milioni 160, hivyo idadi hiyo ni soko kubwa kwa bidhaa
zitakazokuwa zikizalishwa na wananchi.
Kwa upande wake, Rais Kenyatta, alisema, viongozi wa jumuiya hiyo ndio waliofanya kazi ya kulala wakati kumekucha.
Alisema kazi kubwa waliyonayo wao ni kuwaletea maendeleo wananchi kwa kujenga miundombinu.
Aliwataka
viongozi wenzake kubadilika badala ya kuwa na maneno mengi na kwamba
sasa wawe watu wa kazi ambayo itawawezesha wananchi kupata maendeleo na
kuyafurahia.
Magufuli Asema Mafisadi Wakimshinda Asiitwe Rais
Reviewed by The Choice
on
9:50:00 PM
Rating:
No comments: