Kampuni Ya Kichina Matatani Kwa Kutengeneza Vibao Vya Namba Za Magari Kinyume Cha Sheria
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) imefanya msako wa kushtukiza katika kampuni ya
Tanzania China Trade and Tourism Development Ltd iliyoko Barabara ya
Nyerere Dar es salaam baada ya kupata taarifa kutoka kwa msamaria mwema
na kukamata vifaa pamoja na malighafi za kutengeneza na kutoa vibao vya
namba za pikipiki kinyume na sheria.
Katika
msako huo uliofanyika tarehe 19 Februari 2016 katika kampuni hiyo,
Maofisa wa TRA waliweza kukamata na kutaifisha vibao vyenye namba za
pikipiki 2,500 na vibao 5,600 ambavyo havikuwa na namba. Pia maofisa wa
TRA walikamata malighafi za rangi ya vibao katoni tatu, pamoja na
mashine ya kupaka vibao rangi yenye uzito wa kilo 155.
Mashine
nyingine iliyokamatwa katika msako huo ni ya kutengeneza namba za
magari yenye uzito wa kilo 902 ambayo imezuiwa isihamishwe kutoka katika
kampuni hiyo pamoja na kompyuta mpakato ambayo imepelekwa katika
maabara ya uchunguzi TRA kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
Taarifa
za kuwepo kwa utengenezaji wa vibao vya magari kinyume na taratibu na
sheria zilitolewa na msamaria mwema ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa
Kampuni husika Donglinh Guo, Meneja wa Kiwanda Yong Qing Cheng na Meneja
wa ghala Peng Zhan walikamatwa baada ya kutokea fujo wakati wa msako na
kufikishwa katika kituo cha Polisi Changombe.
Kampuni
ya Tanzania China Trade and Tourism Development LTd ndio waingizaji
pekee wa pikipiki za Falcon tangu mwaka 2008 ambapo inatuhumiwa kutoa
vibao vya namba za pikipiki kwa wateja wake kwa shilingi 5,000 kinyume
na sheria.Uchunguzi wa thamani ya kodi iliyopotea bado unaendelea.
Vibao
vya magari na pikipiki hutolewa na kampuni ambazo zinatambuliwa na TRA
baada ya kupewa idhini. Kampuni hizo ni Masasi Sign, Auto Zone, Sign
Industry, Kiboko, Budda Auto works, Parkinson Ltd na Next Telecom.
Ili
kujiridhisha kuwa kadi za pikipiki zinazotolewa kwa wateja wa kampuni
hiyo ni halali, TRA ilifanya uchunguzi na kugundua kuwa kadi hizo
zinatolewa kihalali.
TRA
inawatahadharisha wananchi kufuata taratibu na sheria ili kuepuka
usumbufu unaoweza kutokea endapo watagundulika kujihusisha na vitendo
ambavyo ni kinyume na sheria.
Kampuni Ya Kichina Matatani Kwa Kutengeneza Vibao Vya Namba Za Magari Kinyume Cha Sheria
Reviewed by The Choice
on
10:47:00 AM
Rating:
No comments: