HIVI NDIVYO RAIS .Magufuli Alivyotinga Kivukoni na Magari Yenye Namba za Kawaida Bila Taarifa
Rais John Magufuli ameendelea kufanya ziara za kushtukiza, baada ya
kutembelea ofisi za Kivukoni Dar es Salaam kimyakimya juzi jioni
kuangalia mwenendo wa utoaji huduma za vivuko.
Mashuhuda waliokuwepo eneo hilo Jumapili jioni wakati Rais anafanya
ziara hiyo, walieleza mtindo alioingia nao Dk Magufuli ulikuwa ni wa
kawaida na vigumu kwa mwananchi wa kawaida kung’amu uwapo wa Rais.
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Sharif Mkamba alisema Rais Magufuli
aliingia saa 11 jioni akiwa na msafara wa magari matatu ya kawaida
yaliyokuwa na namba za kiraia.
“Hakukuwa na king’ora chochote kama tulivyozoea bali ulikuwa ni msafara
wa kimya kimya. Aliingia moja kwa moja kwenye zile ofisi na alitumia
kati ya dakika 10 hadi 15 kabla ya kutoka,” alisema Mkamba.
Said Likoko alisema kuwa baada ya kugundua kati ya magari matatu
alikuwepo Rais, walisogea kufuatilia kwa kina kwa kuwa haijazoeleka na
walitegemea huenda baadhi ya watumishi wangewajibishwa.
“Aliteremka na kumuuliza aliyemkusudia na taarifa tulizozipata jana
zinadai hakumkuta huyo bosi, sijui ni meneja au ofisa sisi hatujui,”
alisema Likoko ambaye hujishughulisha pia na biashara ndogondogo eneo la
kivukoni.
Likoko alisema pamoja na kwamba aliingia kimya kimya, Rais Magufuli
hakusita kuwasalimia wasafiri waliokuwa wakisubiri kivuko wakati
alipofanya ziara hiyo.
Alieleza kuwa kama wananchi walifurahishwa na hatua hiyo ya Rais, kwa
kuwa watendaji wengi hawafanyi kazi siku za wikiendi licha ya huduma
zake kufanyika siku zote.
Tangu jana asubuhi kumekuwa na video inayosambaa ikimuonyesha Rais
Magufuli akiwa Kivukoni akitembea kwa miguu ndani ya eneo hilo huku
akishangiliwa na wasafiri waliokuwa wakingoja kivuko.
Hata hivyo, jitihada za kutafuta mamlaka husika kueleza kwa undani
malengo ya ziara hiyo ziligonga mwamba baada ya Katibu Mkuu Kiongozi,
Ombeni Sefue kutopokea simu.
HIVI NDIVYO RAIS .Magufuli Alivyotinga Kivukoni na Magari Yenye Namba za Kawaida Bila Taarifa
Reviewed by The Choice
on
8:59:00 AM
Rating:
No comments: