Polisi Yaua Majambazi Watatu....Baada ya Kupekuliwa Walikutwa na Ujumbe wa Kamanda Suleiman Kova


Watu watatu wanaosadikiwa kujihusisha na vitendo vya kigaidi na ujambazi wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi.

Watu hao walikutwa na karatasi yenye ujumbe kwa aliyekuwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova ulioandikwa:

“Nasaha kwa Kova, mzee andaa kamati ya mazishi ya vipolisi vyako tukiwamaliza tutakufikia wewe.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa tukio hilo, lilitokea Jumamosi iliyopita, eneo la Fire, jijini Arusha wakati mtuhumiwa Athumani Kassim alipokamatwa eneo la Engosheraton akiwa na silaha na aliwataja wenzake.

Kamanda Sabas alisema walipopata taarifa kutoka kwa raia wema walio tilia shaka mwenendo wa mtuhumiwa huyo ambaye alipokamatwa, alikutwa na milipuko, makoti makubwa mawili na kofia ya kuficha uso.

“Baada ya mahojiano, alituambia kuna wenzake wawili anashirikiana nao kufanya uhalifu na tuliweka mtego.

“Saa 5 usiku, askari wetu wakiwa wameambatana na Kassim, walipofika jirani kabisa na nyumba hiyo eneo la Fire, alitoa ishara na wenzake wakaanza kuwashambulia polisi kwa risasi,” alidai kamanda huyo.

Hata hivyo, Sabas alisema polisi waliwazidi nguvu na kuwajeruhi wawili kati yao.

Hata hivyo, magaidi hao walimpiga mwenzao risasi na wao walifariki dunia walipokuwa wakipelekwa hospitali.

Alisema kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi, walikuta vitu mbalimbali ikiwamo sare tano za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kofia tano za kuficha nyuso, vazi moja la karate, pikipiki moja iliyobomolewa na imebandikwa namba bandia.

Alivitaja vitu vingine kuwa ni bendera mbili nyeusi zenye maandishi ya Kiarabu zinazotumiwa na makundi ya kigaidi.

Vitu vingine ni kisanduku cha chuma na hati ya kusafiria ya Abrahaman Athuman Kangaa, iliyotolewa Aprili 2, 2013, simu tano za mkononi na kati ya hizo, moja ilitambulika kuwa ni ya marehemu Mary Joseph aliyefariki kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana Februari 20, mwaka huu, eneo la Engosheratoni pamoja na kifurushi cha unga wa baruti na jambia moja.

Miili ya majambazi hao imehifadhiwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya utambuzi. 
Polisi Yaua Majambazi Watatu....Baada ya Kupekuliwa Walikutwa na Ujumbe wa Kamanda Suleiman Kova Polisi Yaua Majambazi Watatu....Baada ya Kupekuliwa Walikutwa na Ujumbe wa Kamanda Suleiman Kova Reviewed by The Choice on 6:41:00 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.