MWALIMU APIGWA RISASI DAR NA KUFARIKI HAPO HAPO
DAR ES SALAAM: Mwalimu wa
Shule ya Msingi Msigani, Kimara wilayani Kinondoni jijini Dar, Grace
Benedicto 32, (pichani) ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa
kuwa ni majambazi wakati alipokuwa akijiandaa kwenda kumpokea mume wake
kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
Taarifa kutoka eneo la
tukio zinasema kuwa, mauaji hayo yalitokea saa mbili usiku wa Februari
27, mwaka huu huko Msigani, Mbezi, Dar hatua chache kutoka shule
aliyokuwa akifundishia mwalimu huyo.
mwalimu (2)Kwa mujibu wa
majirani wa eneo hilo, siku hiyo watu watatu walifika kwenye duka la
huduma ya pesa na vocha la mwalimu huyo wakiwa kwenye pikipiki moja,
mmoja wao alitoa shilingi elfu kumi ali apewe vocha, mwingine alihitaji
Luku.
“Lakini ghafla wakamuweka
mwalimu chini ya ulinzi. Hata hivyo, alipambana nao, wakamzidi nguvu na
ndipo mwingine aliyejificha mahali akatoa bunduki na kumfyatulia risasi
mbili mwalimu.
“Risasi moja ilimpiga bega
la kushoto, nyingine tumboni. Alidondoka chini huku akipiga kelele ya
kuomba msaada lakini tulipofika tulikuta wale majambazi wameshakimbia,”
alisema jirani mmoja.
Aliendelea kusema kuwa,
polisi walitaarifiwa na walifika katika eneo la tukio muda mfupi na
kumchukua mwalimu kumkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Kibaha mkoani
Pwani lakini daktari alipomchunguza akagundua alishafariki dunia.
Uwazi lilifika msibani,
Kimara ya Stop Over jijini Dar na kuzungumza na mdogo wa marehemu
aitwaye Benard Benedicto ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Ninachojua mimi siku hiyo
dada alikuwa akifunga duka ili akampokee shemeji uwanja wa ndege lakini
muda mfupi kabla ya kuondoka, ndipo walifika hao majambazi.
“Dada alikuwa akiwasiliana
na mume wake hadi pale mume wake alipozima simu baada ya kupanda ndege.
Aliposhuka na kuwasha simu ili ampigie dada, akapokea taarifa ya mkewe
kupigwa risasi, lakini muda huohuo akapigiwa simu kuwa, amefariki dunia.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo,
Dustan Kuzirwa katika mahojiano na Uwazi ofisini kwake wiki iliyopita
alisema kuwa, wamesikitishwa na mauaji hayo ya kinyama ya mwalimu Grace.
“Mwalimu Grace alikuwa
mchapa kiazi na mwenye ushirikiano mkubwa na wenzake. Alikuwa kitengo
cha kompyuta na alianza kazi mwaka 2006. Tunalaani mauaji hayo na
tunaliomba jeshi la polisi kuwasaka wahusika,” alisema Dustan.
Hata hivyo, mume wa
marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Kimati alipohojiwa alisema
waliomuua mkewe siyo majambazi bali kuna siri nyuma yake. Hakuitaja.
Mazishi ya mwalimu huyo yalifanyika katika makaburi ya Banda la Mkaa, Mbezi Jumatano ya Machi 2, mwaka huu.
MWALIMU APIGWA RISASI DAR NA KUFARIKI HAPO HAPO
Reviewed by The Choice
on
3:16:00 PM
Rating:
No comments: