Madaktari 2 na Wauguzi 4 Wasimamishwa kazi Jijini Mwanza Kwa Kukataa Kumzalisha Mjamzito Ambaye Alijifungua Mapacha Wawili Chooni Wakafariki


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Baraka Konisaga, amemwamuru Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Adam Mgoyi kuwasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi wanne katika Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana iliyopo Kata ya Butimba kwa kushindwa kumuhudumia mama mjamzito aliyefikishwa hospitalini hapo na kusababisha kujifungua watoto mapacha na baadaye kufariki.

Hatua hiyo imesababishwa na tukio la mgonjwa Suzana John (27) mkazi wa Kata ya Mkolani kufikishwa na ndugu zake katika Hospitali hiyo, aliyekuwa mjamzito na kupokelewa na Dk Norin Magesa na Muuguzi, Janet Foya waliokuwa zamu ya usiku siku ya Machi Mosi, mwaka huu majira ya saa 4:00 usiku na kushindwa kumuhudumia zaidi ya kutoa lugha isiyoridhisha, pamoja na uzembe.
Akielezea tukio hilo, mwanamke huyo ( Suzan John ) alidai kuwa alianza kusikia uchungu na kuomba msaada kutoka kwa madaktari na wahudumu wa afya waliokuwa hospitalini hapo bila mafanikio.
 
“Nilifika nikiwa hoi, nikawaambia muda wangu tayari  lakini hawakunisaidia zaidi ya kunitolea maneno machafu.
"Wakati muda ukizidi  kwenda huku nikiwa sipewi huduma yoyote, nilihisi kubanwa haja ndogo hivyo nikaamua kwenda chooni .
Kule chooni mambo yakabadilika ghafla, mtoto wa kwanza akawa keshaanza kutoka.Bahati nzuri mle chooni kulikuwa na beseni
"Nililichukua lile beseni kwa ajili ya kuwaweka watoto huku niwakaita manesi.Manesi hao walikuja wakanichungulia halafu wakarudi. Akaja Nesi mmoja mwanafunzi, akakata kitovu akawaweka kwenye nguo, wakawa wamefariki,” Bi. Suzan alieleza kwa uchungu huku akilia.
Baada  ya mapacha hao kufariki, ndugu wa mwanamke huyo pamoja na wagonjwa wengine walioshuhudia mkasa huo walipandwa na hasira huku wakitaka kuwapiga wauguzi hao.
Taarifa za vurugu hizo zilimfikia DC Konisaga ambaye alifika hospitalini hapo  na kukutana kwa dharula na Mkurugenzi wa Jiji, Adamu Mgoyi, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Nyamagana, Kaimu Mganga Mkuu Mkoa, Uongozi wa Hospitali na baadhi ya ndugu wa mgonjwa Suzana John aliyejifungua watoto mapach.

Katika kikao hicho cha dharura, walipokea maelezo ya pande mbili, kutoka kwa wauguzi na familia ya mgonjwa Suzana, na kupitia taarifa zilizokuwa zimeandikwa na Madaktari wawili waliomuona mgonjwa huyo, ndipo DC Konisaga akamuagiza Mkurugenzi Mgoyi na Kaimu Mganga Mkuu kuwasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi wanne ili kupisha uchunguzi wa kitaalamu juu ya tukio hilo.

Konisaga aliwataja wanaotakiwa kusimamishwa kazi kuwa ni Dk Magesa na muuguzi Foya waliompokea mgonjwa wakiwa zamu ya usiku wa Machi Mosi, mwaka huu na kushindwa kumpatia huduma zaidi ya kumtolea lugha chafu na uzembe huku wakishindwa kutoa maelezo wakati wa kukabidhi majukumu kwa madaktari na wauguzi walioingia zamu ya asubuhi ya Machi 2, mwaka huu.

DC Konisaga pia alieleza kuwa pamoja na kuingia kwa madaktari na wauguzi wa zamu ya asubuhi ya Machi 2, bado hawakumjali na kumhudumia mgonjwa huyo huku baadhi wakitoa lugha zisizo za faraja kwa ndugu wa mgonjwa. 
Hata alipozidiwa na kupewa taarifa na ndugu wa mgonjwa huyo, hawakufika na mara kadhaa walikuwa wakifika na kutoka bila kumudumia pamoja na kumsikiliza akilalamika.

Aliwataja wengine wanaotakiwa kusimamishwa kazi mara moja ni Dk Emiliana Mvungi, wauguzi ni Maria Mkankule, Suzana Sindano na Bibiana Moshi ambao walikuwa zamu na kutomhudumia mgonjwa ambaye alijifungua katika mazingira hatarishi akiwa Hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo amemwagiza Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Rweyendela Onesmo ambaye ni Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa ya Sekou -Toure kupewa maelezo ya kina kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk Nangi William na Mganga Mkuu wa Jiji, Dk John Andrew juu ya kushindwa kuchukua hatua pamoja na kupewa taarifa hizo.

Mulongo pia amemuagiza Dk Onesmo kuunda tume ya uchunguzi itakayoshughulikia suala la tukio hilo na kisha kukamilisha kazi hiyo kwa siku moja na kumpatia taarifa ili hatua kali za maadili ya utumishi wa umma zichukue mkondo wake ili pia kuwezesha kusaidia jinsi ya kuboresha utendaji wa kitaalamu na kitabibu katika hospitali hiyo ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kutokuwa na huduma nzuri kwa wagonjwa
Madaktari 2 na Wauguzi 4 Wasimamishwa kazi Jijini Mwanza Kwa Kukataa Kumzalisha Mjamzito Ambaye Alijifungua Mapacha Wawili Chooni Wakafariki Madaktari 2 na Wauguzi 4 Wasimamishwa kazi Jijini Mwanza Kwa Kukataa Kumzalisha Mjamzito Ambaye Alijifungua Mapacha Wawili Chooni Wakafariki Reviewed by The Choice on 10:33:00 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.