Vigogo Watatu Wanusuru Nyumba ya Dk. Slaa Iliyokuwa Imeuzwa Kwa Mnada Baada ya Kushindwa Kurudisha Mkopo


Vigogo watatu nchini wamejitosa kunusuru nyumba ya ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa kwa kumchangia Sh milioni 300.

Hatua hiyo inaelezwa inatokana na maombi ya mmoja wa watu wa karibu wa Dk. Slaa, kuwaomba vigogo hao kunusuru nyumba hiyo iliyopo Mtaa wa Mtipwa, Mbweni jijini Dar es Salaam, ambayo iliuzwa kwa mnada.

Nyumba hiyo ilinunuliwa kwa mnada mwishoni mwa mwaka jana na mfanyabiashara Hussein Ndama, ambaye aliinunua kwa Sh milioni 110.

Baada ya kuuzwa kwa nyumba hiyo zilianza juhudi kutoka kwa watu waliokuwa karibu na Dk. Slaa kwa kutaka kuikomboa, huku mfanyabiashara huyo akigoma kuiuza kwa bei aliyonunulia na kutaka kuiuza kwa Sh milioni 500.

Taarifa hizo zinaeleza kuwa, wakati vigogo hao wakijitosa, mawakili wa mke wa Dk. Slaa pia walifanya kazi kubwa, ili kurejesha nyumba hiyo mikononi mwa familia ya Dk. Slaa.

Chanzo cha kuaminika kimesema  kuwa, baadhi ya vigogo hao kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), waliamua kuingilia kati na kulazimika kuchanga fedha za kukomboa nyumba hiyo.

“Baada ya taarifa za nyumba kutoka kwa watu wa karibu na Dk. Slaa, viongozi watatu waliingilia kati na kuanza kutoa michango yao ambapo zilipatikana Sh milioni 300.

“Vigogo hawa watatu, wawili ni viongozi wa juu wa chama tawala na mmoja ni kiongozi wa ngazi za juu katika shirika la umma (jina linahifadhiwa), na kila mmoja alitoa shilingi milioni 100.

“… tena hilo halikufanyika hivi hivi ila nguvu kubwa ilitumika kuhakikisha hao viongozi wanawasiliana na Ndama (Hussein), ili kumwomba alegeze msimamo wake kuhusu bei ya nyumba aliyonunua. 
“Baada ya majadiliano marefu, Ndama alikubali ingawa kwa masharti zaidi.

"Wakati hilo likifanyika pia mawakili wa mke wa Dk. Slaa walifanya kazi kubwa ili kuweza kurejesha nyumba hiyo katika mikono ya familia ya Dk. Slaa,” kilisema chanzo .

Chanzo hicho kilisema jitihada za vigogo hao zilimfanya Ndama maarufu kwa jina la ‘Ndama mutoto ya ng’ombe’ alegeze masharti ya kiwango cha fedha alichohitaji na hivyo kukubali dau la Sh milioni 300.

Nyumba ilipotoka
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Chadema, Dk. Slaa na mkewe Josephine Mushumbusi walinunua nyumba hiyo namba 74694, iliyopo katika kiwanja namba 117, kitalu ‘1’ Mbweni JKT.

Nyumba hiyo ilinunuliwa na wawili hao Mei 8, mwaka 2012 kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwa gharama ya Sh milioni 117.859.

Dk. Slaa aliwahi kukaririwa na vyombo vya habari Septemba 4, mwaka jana alipokuwa akitangaza kujitoa Chadema, akimshukuru Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kwa kumsaidia sehemu ya fedha za kununulia nyumba hiyo.

Licha ya sintofahamu hiyo, Dk. Slaa alisema hana ugomvi na Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

“Ninamuheshimu sana Mbowe, sina ugomvi naye maana hata nyumba ninayoishi amehusika kunichangia na hata kunisaidia mambo mengi,” alisema Dk. Slaa.

Jinsi Nyumba ilivyouzwa kwa mnada
Mfanyabishara huyo alinunua nyumba hiyo Desemba 27, mwaka jana kwa mnada uliosimamiwa na kuendeshwa na Dalali wa Mahakama, Bilo Star kwa ajili ya kufidia deni la mkopo wa Sh milioni 52.999 ambalo lilitakiwa kulipwa kufikia Novemba 26, mwaka jana katika Benki ya Equity ya jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa kwamba mke wa Dk. Slaa, Josephine Mushumbusi, ndiye aliyetoa hati hiyo ya nyumba kama dhamana ya mkopo huo uliochukuliwa na mtu anatajwa kwa majina ya Salehe Swedi Nehale wa Kampuni ya ujenzi ya T/A Nehale Building Material Supplies.

Safari ya Nje
Septemba 8, mwaka jana Dk. Slaa, alisema anakwenda Marekani pamoja na familia yake kwa mapumziko.

Akiwa nchini humo kwa ajili ya mapumziko na kujiendeleza katika kozi fupi katika tasnia ya Sheria na Lugha, Dk Slaa alisema nyumba yake itakuwa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi.

Akizungumza katika mahojiano yaliyorushwa kituo cha televisheni cha Azam, mwanasiasa huyo, alisema akiwa mapumzikoni Marekani, nyumba yake itakuwa inalindwa na Jeshi la Polisi kutokana na vitisho ambavyo amekumbana navyo tangu alipoamua kuachia ngazi Chadema.

“Ninatishiwa maisha, ni lazima nichukue hadhari….., ninatishiwa kupigwa mawe.Ni kweli ninalindwa na usalama,” alisema Dk. Slaa akiwa anahojiwa na mwanahabari nguli, Tido Mhando.
Vigogo Watatu Wanusuru Nyumba ya Dk. Slaa Iliyokuwa Imeuzwa Kwa Mnada Baada ya Kushindwa Kurudisha Mkopo Vigogo Watatu Wanusuru Nyumba ya Dk. Slaa Iliyokuwa Imeuzwa Kwa Mnada Baada ya Kushindwa Kurudisha Mkopo Reviewed by The Choice on 10:47:00 AM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.