Mengi yazidi Kuibuka Kuhusu Nyalandu na Kampuni ya Uwindaji Ambayo Majangili Walitungua Helkopta yao na Kuuwa Mzungu


Mambo mapya yameibuka kuhusu kampuni ya Kimarekani ya Friedkin Conservation Fund (FCF) ambayo majangili walidungua helikopta yake mwezi uliopita na kusababisha kifo cha rubani raia wa Uingereza, Roger Gower.
FCF inamiliki kampuni tanzu za uwindaji wa kitalii za Mwiba Holdings Ltd, Tanzania Game Trackers Safaris (TGTS) Ltd na Wengert Windrose Safaris.

Wakati helikopta hiyo ikidunguliwa kwa kile kinachoelezwa kwamba ilikuwa kwenye doria dhidi ya majangili, kumbukumbu zilizopo Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonesha kuwa kampuni ya Mwiba Holdings Ltd ni miongoni mwa watuhumiwa wa ujangili
Uchunguzi unaonesha kumekuwapo matukio kadhaa ya wafanyakazi wa Mwiba kukamatwa wakiwa wameua wanyamapori na kukutwa na nyara za Serikali.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii vimesema mara zote kesi zinazoihusu kampuni hizo zimekwama kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni urafiki wao wa karibu na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Nyalandu.

Urafiki wa Nyalandu na wamiliki wa kampuni hizo ulikuwa mkubwa kiasi cha kumpatia moja ya helikopta zake aitumie kwenye mbio za kuwania urais, kabla ya kushindwa na kujielekeza kwenye ubunge. Helikopta iliyodunguliwa na majangili ndiyo aliyoitumia wakati wote wa kampeni zake za ubunge

Nyalandu alimwamuru Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa wakati huo, Paul Sarakikya, kutoa Leseni ya Rais kwa familia ya Tom Friedkin (mmiliki wa kampuni hizi) kuwinda wanyamapori 700 katika vitalu vinane na eneo la wazi la Makao. Leseni hizo zilitolewa bure bila kulipiwa hata senti.
Miongoni mwa wanyamapori waliokuwa kwenye orodha ya kuuawa ni tembo walio katika hatari ya kutoweka.

Pia Nyalandu alikiuka sheria kwa kupuuza ukomo wa idadi ya vitalu vitano kwa kampuni moja. TGTS imemilikishwa vitalu vinane pamoja na eneo la wazi; hali ambayo ni ukiukwaji wa kifungu cha 38(7) cha Sheria ya Wanyamapori.
Kampuni hiyo pia ilipewa vitalu na Nyalandu kinyemela, ilhali sheria ikiagiza kuwa kitalu kinapobaki wazi sharti kitangazwe kwanza na waombaji washindanishwe katika mfumo na utaratibu ulio wa haki na uwazi [Kanuni ya Uwindaji wa Kitalii 18(1).

Pamoja na kutoa Leseni ya Rais, Wamarekani hao walileta watoto wadogo, chini ya umri wa miaka 18 kuwinda; jambo ambalo ni kinyume cha kifungu cha 43(3) cha Sheria ya Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.
FCF na kampuni tanzu imekuwa ikiendesha shughuli za utalii kwenye eneo la Makao WMA tangu 2011 baada ya Mwiba Holdings Ltd kumilikishwa eneo jirani na WMA ya Makao kwa ajili ya shamba la mifugo na wanyama (Makao Ranch).

Kampuni ya Mwiba Holdings Ltd chini ya TGTS Ltd ambazo zinamilikiwa na Friedkin Conservation Fund (FCF) imekuwa ikiendesha shughuli za utalii kwenye eneo la Makao WMA tangu 2011 baada ya Mwiba Holdings Ltd kumilikishwa eneo jirani na WMA ya Makoa kwa ajili ya shamba la mifugo na wanyama.
Hata baada ya kumalizika Mkataba wake na JUHIWAPOMA, kampuni ya Mwiba Holdings Ltd iling’ang’ania na kuendelea kukalia eneo la Makao WMA kwa mabavu na kinyume cha sheria.

Source:Jamhuri
Mengi yazidi Kuibuka Kuhusu Nyalandu na Kampuni ya Uwindaji Ambayo Majangili Walitungua Helkopta yao na Kuuwa Mzungu Mengi yazidi Kuibuka Kuhusu Nyalandu na Kampuni ya Uwindaji Ambayo Majangili Walitungua Helkopta yao na Kuuwa Mzungu Reviewed by The Choice on 9:28:00 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.