MBUNGE WA CHALINZI MH RIDHIWANI KIKWETE AKANA TAARIFA KUMILIKI KAMPUNI YA LUGUMI

MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amekanusha taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii na kwenye vyombo vya habari kuwa yeye ni mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Lugumi, inayodaiwa kupewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole kwenye vituo vya Polisi.Ridhiwani ametajwa katika habari hizo kuwa ni mmiliki wa kampuni ya Lugumi pamoja na wamiliki wengine ambao ni Said Lugumi na aliyekuwa mkuu wa Jeshi la Polisi, Said Mwema.Akizungumza na gazeti hili, Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alisema yeye hahusiki na kampuni yoyote ya Lugumi ingawa wana urafiki wa kawaida na mmiliki wa kampuni hiyo.


“Kwanza kabisa mimi si mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo, hilo ni jambo la msingi kabisa watu waelewe na sijawahi kufanya biashara yoyote na Lugumi. Said Lugumi ambaye ni mmiliki wa kampuni hiyo tunafahamiana naye na ni rafiki yangu,” alisema Ridhiwani.

Ridhiwani alisisitiza kuwa hana uhusiano wa kibiashara na mtu huyo na kwamba hafahamu ni kwa nini amehusishwa na kampuni ya Lugumi.

“Hapa ni watu tu wanaamua kuingiza tu maneno yao, haya maghorofa ninayotajwa kumiliki Dar es Salaam hata sijawahi kutembelea ujenzi wake, wameamua kuniingiza, Lugumi nafahamiana naye binafsi tu lakini wananiingiza,” alisema Ridhiwani.

Alisema jambo hilo bado liko ndani ya Kamati ya Bunge na baadae ameliona kwenye magazeti ya juzi kuwa Jeshi la Polisi litatoa taarifa yao, hivyo asingependa kulizungumzia kwa undani. Hivi karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilitoa siku saba kwa Jeshi la Polisi nchini kupeleka mkataba walioingia baina yao na Kampuni ya Lugumi.

Kamati hiyo ilipokutana na Jeshi hilo kupitia taarifa ya hesabu zao za mwaka 2013/14 zilizokaguliwa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly alisema jeshi hilo

mwaka 2011 liliingia mkataba na kampuni hiyo kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya Polisi vya wilaya nchi nzima ambavyo viko 108.

Alisema mkataba huo ulikuwa wa Sh bilioni 37 pamoja na kodi na kwamba hadi sasa kampuni hiyo imeshapewa asilimia 99 ya fedha zote ili hali vituo vilivyofungwa mashine hizo ni 14 tu, kati ya vituo vyote 108.

Ridhiwani alisema angependa jamii ifahamu kuwa hana uhusiano na kampuni hiyo kwa kuwa hafahamu kabisa hata malipo yaliyofanywa kati ya Serikali na kampuni ya Lugumi anasikia tu kama ambavyo watu wengine wamesikia.

Chanzo: Habarileo
MBUNGE WA CHALINZI MH RIDHIWANI KIKWETE AKANA TAARIFA KUMILIKI KAMPUNI YA LUGUMI MBUNGE WA CHALINZI MH RIDHIWANI KIKWETE AKANA TAARIFA KUMILIKI KAMPUNI YA LUGUMI Reviewed by The Choice on 10:39:00 PM Rating: 5

No comments:

Powered by Blogger.